Watu wengi wamekuwa wakijifunza meditation tangu karne na karne, miaka na miaka. Sio kitendo kilichoanza hivi sasa bali ni kitendo kilichoanza tangu zamani na kimekuwa na faida mbalimbali kwa watu waliojifunza na kufanya taamuli. Wengine ni kutokana na kupunguza stress, kujifunza kuongoza akili zao, kuachana na mazoea wanayoshindwa kuyaacha na kutokana na kuongeza hekima ya kiimani.
Ningependa kuelezea faida chache nzuri ambazo zinapatikana pale mtu anapofanya taamuli vyema na kwa mara kwa mara.
1. Taamuli (Meditation) inasaidia kutengeneza furaha ya ndani.
Tunaposema furaha ya ndani tunamaanisha nini? Ni furaha unayotembea nayo wakati wote, ni furaha isiyotegemea maisha yako yapoje, ni furaha isiyotegemea una vitu gani bali ni furaha inayopatikana ndani mwako. Wengi hupata furaha kutokana na hali na vitu, na kipindi cha wakati mgumu wao hukosa furaha kwani furaha yao inategemea vitu vya nje ambavyo havidumu milele. Lakini katika meditation unajifunza kuachana na kujishikilia na mawazo, fikra, hisia, na milango ya ufahamu. Unajifunza kuingia ndani na kutafuta kisicho na mwanzo wala mwisho. Ambacho wakati wowote upo nacho. Nacho kinakuunganisha source/chanzo na ufahamu mkuu wa Ulimwengu ambao wakati wote mpo pamoja.
2. Taamuli (meditation) husaidia kujifunza ku-ufurahia wakati uliopo.
Badala ya kupambana na watu na hali meditation inakusaidia kuwa mtulivu na mkimya na kutazama hali, watu na vitu katika hali ya busara na hekima kwani unajifunza kuongoza akili yako vyema. Tatizo likitokea badala ya kuwaza vibaya unajikuta unatafuta njia sahihi ya kusuluhisha na kuweza kuwaza kiusahihi. Hujifunza kutojishikilia na hali na mawazo hivyo hali fulani ikitokea unakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yako upendavyo na sio katika kuongozwa na akili yako bila wewe kujijua
3. Husaidia kuongeza umakini.
Katika meditation mtu hujifunza kuweka akili yake katika eneo moja. Mfano kuweka akili kwa jinsi pumzi inavyopanda na kushuka. Ni kitendo kigumu kujizoesha kuweka akili katika kitu kimoja kwani muda wote akili huama sehemu moja kwenda nyingine, lakini kwa kujizoesha na kuweza kuweka akili sehemu moja utaweza kuiongoza akili yako vyema na kwa nguvu sana. Akili ina nguvu sana, akili isipothibitiwa itakutawala bila wewe kujijua. Mfano Mbwa anayegongewa kengele kabla ya kula, akizoeshwa baada ya muda hata ukimpigia kengele atakuja kwa akili yake imeshajiweka hivyo na inamuongoza hivyo bila hata yeye kujifahamu kwa kuona ni kawaida. Kutokana na kuweza kujiongoza vyema unakuwa na ubora katika kuweka umakini katika unachofikiria na unachokifanya kiusahihi zaidi, kwani akili yako yote inakwepo kwenye sehemu moja. Na pia nguvu ya akili inakuwa kubwa katika kutafakari na kuweka ufahamu.
4. Hautakuwa mtu wa kuchukizwa na vitu vidogo vidogo.
Kama ulikuwa mtu wa hasira sana, chuki sana, mbinafsi, unayewatazama watu vibaya na kadhalika, ukifanya taamuli kwa muda mrefu utajikuta unaachana na mambo unayoona hayana umuhimu, na unakuwa mwepesi kufanya maamuzi yanayohitaji nia yenye nguvu. Mfano unaweza kuamua kuacha mazoea ambayo ulikuwa unaona ni vigumu, unaweza kuachana na fikra na mawazo yasiyo sahihi na hii ni kutokana na kuwa unaweza kuiongoza akili yako utakavyo.
5. Husaidia kujifunza kujali, kusamehe, na kujali watu.
Taamuli huweza kubadili kabisa saikolojia ya mtu na jinsi mtu anavyotazama na kutenda katika maisha yake. Ukifanya meditation (taamuli) sana unakuwa hauna hasira kabisa. Hasira unaweza kuithibiti ikianza na unaepuka mazara ya hasira. Utajikuta haufanyi maamuzi yako ukiwa na hasira, unakuwa makini, tulivu na mwenye amani. Ukiweza kufanya maamuzi katika hali isiyo na hasira na chuki na ubinafsi itakusaidia kuweza kuongeza tabia ya kujali wengine, kutambua hali za wengine, kusamehe kirahisi bila kuumia na chochote na pia inasaidia kutambua hali za watu kiundani kwani akili yako inakuwa tulivu na yenye nguvu kupelekea kuweza kuzitambua akili za wengine na kuelewa hali zao kwa kina.
6. Unaanza kuhisi uzima na unaufurahia uhai.
Utajikuta unapata furaha kwa vitu vidogo tu, unajikuta hauweka mawazo yako kwenye taabu na upande mbaya wa maisha, unajikuta hauna hasira, chuki na ubinafsi, unazidi kuwa makini na jinsi maisha yanavyokuendea, unaona kila ncha ya nafasi iliyopo katika maisha na kutambua umuhimu wake, unaanza kufahamu hali za watu na kukusaidia kuishi nao vyema, unajifunza kutumia akili yako, fikra yako, imani yako, mawazo yako na ufahamu wako katika kuumba na kubadili uhalisia wako wa maisha. Pia inakuunganisha na Ufahamu Mkuu (Wengine humpa jina la Mungu) na kutambua maajabu ya maisha na kuweza kusikiliza sauti ya nafsi itokayo kwake.
Kuna faida nyingi sana na nyingi zinaleta faida katika upande wa faida nyingine. Kila faida inaunganisha faida nyingine hivyo hutaweza kufika mwisho. Kuna faida za kisaikolojia, faida za kiafya, faida za kiimani, faida za kisayansi na kadhalika lakini zote hizi zinaashiria kuwa jamii ingekuwa inajifunza Taamuli ingeweza kufika mbali sana kwani Taamuli imewasaidia wengi ulimwenguni walioweza kutimiza malengo yako kiimani na kimaisha.
| 1:42 PM
0 comments: