Wednesday, September 23, 2015

Shoga, Uonjwe We Pombe Ya Kienyej

Jamani hebu nitumieni basi mvuke salama, hivi muoaji wa kweli humuonja mwanamke ndipo amuoe kweli? Mmh! Simpendi jamani mwanamke kugeuzwa chungu cha mboga kuingiza mkono na kuonja. Utaonjwa na wangapi mwisho wa siku unabaki kituko cha mtaa.

Najua utashangaa kuona nimeanza na gia kubwa bila hata kutanguliza salamu, kwa kweli jambo linaloniudhi salamu kwangu si muhimu, kama kulizungumzia lililouchefua moyo wangu. Juzi nilipata malalamiko, msichana mmoja aliyefuatwa na mwanaume mtu mzima ambaye ni mume wa mtu na kumuomba awe mkewe kutokana na mkewe kuwa na matatizo ambayo siwezi kuyaweka gazetini.
Kwa kweli mwari huyu alitatizika kuolewa ukewenza kuhofia kujiingiza katika vita ya ndani, lakini yule mwanaume alimuhakikishia kuwa kuoa mke mwingine alipata ruksa kutoka kwa mkewe. Mtoto wa kike kiguu na njia mpaka kwangu na kuniuliza akubali au akatae.
Kwa vile najua ukewenza si dhambi nilimweleza akubali. Baada ya hapo tulipoteza na kuonana juzi akiwa anatokwa na michozi tikwatikwa.He! Mwari kulikoni? Nilimuuliza, jibu eti tangu wakati ule ndoa imekuwa kitendawili, kauli ile ilinishtua na kuuliza bado anaye? Jibu, ndiyo. Nilishangaa kasi ya awali na kuamini ndoa ingekuwa ndani ya wiki, lakini umevuka mwaka.
Mmh! Mtoto wa kike niliinama chini kuwaza na kuwazua ili kutaka kujua sababu ya mwari wangu kuiona ndoa kama daladala inayopita mbele yake kwenda na kurudi, kazi iliyomshinda Alawa. Kwa vile mimi ni nyani mzee niliyepita mapori mengi nilipata jibu na kumuuliza swali.
Tangu wakati ule umeshamuonjesha mwili wako? Jibu lilikuwa lilelile nililowaza kuwa alimpa baada ya msimamo wa muda mrefu na kuamini kumvulia nguo ya ndani ingeharakisha ndoa kumbe siyo. Siku zote huwa sipendi kumlaumu mtu kwa kosa alilolifanya kwa bahati mbaya, lakini huwa simpendi mtu anayerudia kosa moja mara mbili kama mnyama na mwisho wa siku aombe ushauri, haipendezi.
Jamani wari wangu, mimi anti yenu nimeamua kutoa elimu ya bure kupitia gazeti hili kwa nini msiichukue. Usiniangalie mimi, angalia ninachokueleza ambacho huwa ni faida kwenu. Jamani hebu basi tuwe na msimamo kujitoa kimwili si njia ya kuharakisha ndoa bali kujidhalilisha.
Mwanaume kama kweli anakupenda na kutaka uwe mwenza wake, kwa nini awe na haraka ya kutaka kukuonja kwanza? Sasa umeonjwa na kuonekana si mtamu ndiyo uachwe? Kwa mtindo huo utaonjwa na wanaume wangapi.
Mila na desturi yetu Waafrika ni kuchunguza tabia ya mtu si kuujua utamu wake, jamani haya yametoka wapi kuonjwa ndipo uolewe? Umekuwa pombe ya kienyeji?
Nawaasa wanawake wanaojiandaa kuolewa au kuwa na wachumba wasitoe miili yao ovyo, kama wanataka kuitumia wataipata baada ya ndoa, lakini wakijiroga kuitoa basi wajue itakula kwao, watatumiwa na mwisho wa siku kutupwa kama mpira wa kiume uliotumika.

Author:

0 comments: