Saturday, November 28, 2015

Sasa Tunakwenda Kushuhudia Tofauti ya UKAWA Kushika Dola na CCM Kurudi Madarakani

Tutakachoshuhudia katika awamu hii ni kuibuliwa kwa madudu makubwa huku wakuu wa mashirika ya umma wakiwajibishwa kama mbuzi wa kafara lakini vigogo walioko kwenye system wakipeta au wakikamatwa wale dagaa tu.

Inawezekana kabisa,hawa wakuu wa mashirika haya ya umma walikuwa wanafanya kazi tu ya kulinda maslahi ya wakubwa na huenda wao wakawajibishwa huku vigogo hawa wakiachwa jambo ambalo serikali ya UKAWA isingelifanya.

Kumekuwepo na madai/tuhuma za vigogo kutumia majina ya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kuendesha biashara zao kitu ambacho sidhani kama serikali ya Magufuli itathubutu kukufanyia uchunguzi-UKAWA wangethubutu.

Hivi biashara ya madawa ya kulevya, magogo,meno ya tembo na hata hii ya kupitisha makontena kiholela bandarini haina baraka za wakubwa?Magufuli ataweza kuwawajibishi vigogo hawa pindi wakibainika?

Fukuafukua hii ya serikali ya Magufuli huenda ikawa "counter-productive" kwa CCM na serikali yake na jambo hili likiwa handled vibaya, huenda likafanya watu waichukie zaidi CCM badala ya kuipenda kama wengi wanavyodhani.

Anachokifanya hivi sasa Magufuli ni sawa kuwadhihirishia watanzani,tena kwa ushahidi, ni kwanini CCM haikupaswa kuchaguliwa kurudi madarakani na akishindwa kuwawajibisha vigogo watakaobainika atakuwa anajimaliza mwenyewe.


Hivi sasa UKAWA wamerahisishiwa kazi kwani karibu kila kitu kinaibuliwa na serikali yenyewe na wao kama wapinzani watakuwa na kazi ya kushinikiza hatua zichukuliwe jambo ambalo nina mashaka kama litatekelezwa kwa uaminifu hata kama itaundwa hiyo Mahakama ya Mafisadi.

Bungeni ndio kutakwenda kuchafuka na hapa ndio mtihani wa Magufuli na serikali yake kuchukua hatua utakuwa mgumu zaidi maana ndani ya bunge huenda yakaibuliwa mengi ambayo hatukuyatarajia.

Kwa mfano, yanayosemwa na watu na kuandikwa mitandaoni kuhusu kampuni ya Home Shopping Center huenda yakaibukia Bungeni na wabunge wa UKAWA wakadai uchunguzi ufanyike kuhusu kampuni hii.

Kufichua tuhuma na watuhumiwa ni jambo moja, na kushughulikia tuhuma na watuhumiwa ni jambo lingine.

Kwenye orodha hakuna wafadhili?

Tusubiri.

Source: By Salary Slip/Jamii Forums

Author:

0 comments: