Meneja wa muziki hapa Bongo, Ostaz Juma Namusoma.
Musa mateja
UKIANZA kutaja majina ya mameneja
mbalimbali wa muziki hapa Bongo, baadhi ya majina makubwa yasiyoisha
miongoni mwao huwezi kulikosa jina la Ostaz Juma Namusoma.
Kwa mujibu wa kinywa chake mwenyewe Ostaz Juma Namusoma, juzikati
nilipata nafasi ya kumbana na kunieleza kiunagaubaga namna alivyoweza
kujipenyeza hadi kupata jina kupitia muziki wa Bongo.
Kwa kinywa chake aliniambia kwamba,
muziki kwake ni sehemu ya maisha ambayo ameishi kwa kipindi kirefu sana,
kwani tangu alipokuwa mdogo alipenda muziki kushinda kitu chochote,
msikie mwenyewe.
OSTAZ JUMA: Mimi ni miongoni mwa vijana
wa kipindi hicho ninayetokea Musoma mkoani Mara. Nilianza kupenda muziki
tangu nasoma shule ya msingi tena mapema kabisa nikiwa darasa la tatu.
Nikiwa shuleni nilikuwa napenda sana
kuimba nyimbo mbalimbali za wasanii wa Kongo hadi nikafikia hatua ya
kununua redio na kuwarekodi watoto wenzangu wakiimba kisha nazitunza
nyimbo walizokuwa wakishindana kuimba hasa za Boringo za Wazaire.
Nimefanya hivyo hadi nikawa nagombezwa
na wazazi wangu lakini sikukoma hadi nilipokuwa mtu mzima na kuanza
kujifanyia mambo yangu ambapo wazazi hawakuweza kuniingilia.
Kwa jinsi hii ndiyo utaweza kugundua
kuwa nina kipaji cha kusimamia watu ndiyo maana nimeweza kuwasaidia
wanamuziki wengi tu kwenye dansi ambapo kabla ya kujiingiza katika Bongo
Fleva niliwahi kuwasaidia wanamuziki wa dansi kama Ally Chocky, Super
Nyamwela, Jose Mara, Kalala Junior, Nyoshi El-Saadat, Mwinjuma Muumini
na Mulemule.
Tabia za wanamuziki kiukweli hazipishani
sana hivyo ukiona meneja yeyote analalamika juu ya wanamuziki basi ujue
matatizo yao mara kadhaa yamekuwa hayapishani sana, ila wanaopishana
tabia na namna ya kuongoza ni mameneja tu.
Namna ya kuongoza na kummeneji mtu
kunategemeana na uwezo wa kifedha na akili pia, nasema hivyo kwa sababu
muziki wetu umekuwa ukiyumba mara kadhaa kutokana na baadhi ya mameneja
kuwa wasimamizi wabovu na wengine wanasimamia wakiwa hawana fedha ya
kuweza kuwaongoza wasanii.
Meneja ninayeweza kumpa saluti hapa
Bongo ni Saidi Fella kwani ameonesha njia kubwa ya kuimarisha Muziki wa
Dansi na sasa umeanza kuwa juu kiasi cha watu kuanza kuupenda tofauti na
kipindi cha nyuma ambapo ulianza kupoteza dira.
ALIANZAJE KUSIMAMIA BONGO FLEVA?
Ostaz Juma: Kwenye Bongo Fleva niliingia
baada ya kuanza kumsimamia shemeji yangu aitwaye Abdallah David
aliyekuwa akijiita Fil David, huyu nilijikuta namsimamia baada ya
kumuona ana kipaji kizuri na baadaye nikaanzisha rasmi kampuni yangu ya
Mtanashati.
Mtanashati ilipoanza tu nikapunguza
kuwasaidia wanamuziki wa dansi hivyo nikajikita kwenye Bongo Fleva
ambapo nilianza kumsimamia marehemu Sharo Milionea aliyemleta Kitale,
lakini kabla sijaingia mkataba na Sharo akafariki dunia.
Baada ya kufariki kwa Sharo Milionea
ambaye ndiye msanii naweza kujisifia katika upande wa Bongo Fleva kwa
kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana, nilimchukua PNC, Dogo Janja na
Happy Balis ambao nilifanyanao project kibao kiasi ilifikia hatua nikawa
nakosana hadi na mke wangu kisa muziki huu.
Nimekuwa nikiwasaidia wasanii hawa kwa
muda lakini nilichoweza kujifunza ni kwamba wasanii wengi hawana adabu
kabisa, kwani kuna siku niliwahi kukosana na mke wangu kwa kushindwa
kumpeleka hospitali kisa kumpeleka Dogo Janja kwenye interview jambo
ambalo mke wangu amekuwa akinikumbusha kila mara nami huwa halitoki
kichwani hadi leo.
Fedha niliyowahi kutumia hadi leo kwa
ajili ya Dogo Janja na PNC naweza kujenga hata ghorofa tatu hapa mjini,
lakini kwa kuwa nilikuwa naupenda muziki ndiyo maana leo utaona inafikia
muda sasa nimeamua kuachana na hawa Bongo Fleva maana hawana nidhamu
hata tone ila ukilinganisha na wanamuziki wa dansi utagundua ni bora
dansi kuliko Bongo Fleva.
Nasema wanamuziki wa dansi ni bora
kuliko wa Bongo Fleva kwa sababu wakati nadili na wanamuziki wa dansi
walikuwa wanaonesha nidhamu ya hali ya juu jambo ambalo wanalifanya hadi
sasa.
Ujue nilikuwa nikiwapatia fedha za kodi
za nyumba, mara nyingine kama Christian Bella na Chocky hawa niliwahi
hata kuwalipia studio mara kadhaa kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao
binafsi.
Christian Bella yeye aliwahi hadi
kunitungia wimbo ambao unaitwa Ubinadamu ambao hata yeye ukimuuliza leo
anaujua na ninao mimi mwenyewe.
Wasanii wakijua kuwa muziki ni kazi na
sehemu ya maisha yao basi hakuna Bongo Fleva atakuja kushindwa kufanya
mambo makubwa kama anavyofanya Diamond kwani kinachomfanya kuheshimika
na kufanikiwa ni nidhamu yake tu.