Brez News Blog
MSHAMBULIAJI wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika timu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta amesema iwapo ataondoka katika timu hiyo hana mpango wa kucheza katika timu yoyote Afrika.Akizungumza Dar es Salaam juzi Samatta alisema hatarajii kucheza timu nyingine iwe Afrika Kusini au nchi yoyote ya Afrika zaidi amelenga Ulaya ambapo amekuwa akipata mialiko mingi ya kwenda kufanya majaribio.
Samatta, ambaye ameondoka na kikosi cha Taifa juzi kwenda Ethiopia kwa ajili ya kambi alisema amekuwa akipata simu nyingi kutoka kwa mawakala wa Ulaya hivyo anategemea baada ya TP Mazembe atakwenda kucheza Ulaya.
“Barani Afrika hakuna timu kubwa kama TP Mazembe hivyo nitakapoondoka kule manaake nataka nikacheze Ulaya na baada ya miaka 20 nitakuwa nimefikisha kile ninachokikusudia,” alisema.
Alizungumzia kuhusu kushindwa kwenda kucheza Urusi Samatta alisema ni kwa vile hakutimiza kile alichokusudia.
Alisema alitakiwa akacheze siku saba lakini alicheza siku tatu kisha akaumia kifundo cha mguu hivyo alitakiwa akapumzike kwa siku 10 na wakati huo akiwa bado hajatimiza zile siku kwa ajili ya kutathminiwa.
Mchezaji huyo alisema anatarajia siku moja ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa Ulaya itatimia kwani ataendelea kuonesha uwezo wake.
0 comments: