Saturday, September 19, 2015

Mabango ya Lowassa yazua kizaazaa

MABANGO yenye picha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, yanayoendelea kubandikwa katika maeneo mbalimbali nchini yamezua kizaazaa, baada ya mengine kuondolewa na wale wanaofanya kazi ya kuyaweka kutishwa na hata kuwekwa ndani na Jeshi la Polisi.
Hali hiyo imejitokeza mkoani Iringa, ambako vijana wanaofanya kazi ya kuweka mabango hayo waliwekwa ndani na Jeshi la Polisi na jijini Dar es Salaam ambako bango lililokuwa limewekwa katika Soko la Kariakoo liliondolewa saa chache tu baada ya kubandikwa na hivyo kuzua mjadala kila kona.
Wakati wale waliokamatwa mkoani Iringa wakidaiwa kuwekwa ndani pasipokuwa na sababu yoyote hadi pale walipotolewa na maofisa wa Chadema, Jijini Dar es Salaam bango hilo liliondolewa na uongozi wa Soko la Kariakoo kwa madai ya kubandikwa kimakosa.
Juzi saa 12 jioni wafanyakazi wa kampuni ya Platnum Media Co. Ltd walifika sokoni hapo na kuanza kubandika bango hilo lililokuwa na picha ya Lowassa, ikiambatana na maandishi yanayosomeka; ‘Edward Lowassa…Ni wakati wa mabadiliko’.
Wakati bango hilo likibandikwa umati mkubwa ulikusanyika karibu na eneo hilo na kuanza kushangilia, huku wengine wakiimba “Rais…rais…rais”.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Meneja wa Soko la Kariakoo, Florens Seiya, alisema yeye ndiye aliyetoa amri ya kuondolewa kwa bango hilo kwa kuwa soko hilo ni taasisi ya umma na hairuhusiwi kuwekwa mabango ya kampeni.
“Ni kweli tunamfahamu aliyebandika bango hilo, ni mtu ambaye tuna mkataba naye wa kutumia ubao huo kubandika mabango, lakini hili lilibandikwa kimakosa bila kutushirikisha,” alisema Seiya.
Alisema katika mkataba wa soko hilo na kampuni ya Platnum Media Co. Ltd, kifungu cha sita kinamtaka aonyeshe maudhui yaliyomo katika mabango kabla ya kubandika, kitu ambacho yeye (Platnum) hakufanya.
“Jana (juzi) baada ya kufunga ofisi na kuondoka ndipo alipofika na kuanza kuweka bango hilo, jambo lililofanya watu wakusanyike kwa wingi utafikiri pana mkutano wa siasa huku wengine wakishangilia,” alisema Seiya.
Alisema kutokana na soko hilo kuwa ni taasisi ya umma, hairuhusiwi kuweka tangazo lolote linalohusu kampeni za kisiasa kwa kuwa wao hawafungamani na chama chochote.
“Hebu angalia mwenyewe (huku akionyesha rekodi ya video ambayo inaonyesha watu walivyojaa huku wakishangilia wakati bango hilo likiwekwa) nani angeweza kuilinda amani mahali hapa,” alisema.
Aliongeza kuwa hata hivyo, wamemwandikia barua mteja wao huyo, Platnum ajieleze kwa nini alivunja kifungu hicho kinachomtaka apeleke maudhui kabla ya kubandika chochote.
“Kifungu cha sita cha mkataba kinasema kuwa soko la Kariakoo lina haki ya kukataa matangazo yasiyoruhusiwa kisheria na tamaduni za nchi… hawa Platnum tunafanya nao biashara kwa takribani miaka nane na hajawahi kubandika chochote bila sisi kukiona,” alisema Seiya.
Mtanzania imeonyeshwa barua hiyo yenye kumbukumbu namba SKM/B/125 iliyokuwa na kichwa cha habari ‘ukiukaji wa mkataba wa matangazo’ ya Septemba 4 mwaka huu, iliyomtaka Platnum ajieleze.
Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo walisema kuwa hizo ni njama za wana CCM kwa kuwa watu walijaa na kushangilia sana.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Hamisi Napinda, alisema saa 12 jioni wakati bango hilo likiwekwa, polisi walifika muda huo huo na baada ya wao kuondoka tu wakaliondoa.
“Jana (juzi) muda mfupi baada ya kubandikwa bango la Lowassa askari walifika na difenda mbili walipoondoka tu likabanduliwa, hii ni hujuma wanazomfanyia,” alisema Napinda.
UKAWA KUSHITAKI
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kufanya siasa za uchochezi na badala yake wafanye siasa safi zinazojikita katika hoja.
Umoja huo pia leo unatarajia kuwasilisha andiko la kisheria kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) ambalo litakuwa na malalamiko kuhusu matukio na hujuma zinazoendelea katika kipindi hiki cha kampeni.
Tupe maoni yako hapo chini

Author:

0 comments: