Hata hivyo, wakati serikali ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa, ikiendelea kutafuta suluhu ya kudumu kuhusiana na ukwepaji kodi, imebainika kuwa kazi hiyo siyo lelemama kwani zipo njia zaidi ya tisa zinazotumiwa kukwepa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mosi, ni kupitia mwanya utokanao na mfumo wa zamani wa malipo usiohusisha ule wa sasa wa kielektroniki, maarufu kama ‘E-Payment’.
Kwamba, wafanyabiashara wengi hutumia mfumo huo wa zamani unaohusisha matumizi ya karatasi zilizojazwa kwa mkono na hivyo kuwezesha ujanja wa kubadili taarifa kwa manufaa ya mitandao ya wakwepaji wa kodi.
“Tatizo lililopo ni kwamba mfumo wa E-Payment ni mpya (umeanza Julai) na umefungwa kwenye benki moja tu iliyopo ndani ya eneo la Bandari… ule wa zamani unaendelea kutumiwa na wajanja hucheza na maandishi ya kujaza kwa mkono kuhujumu mapato ya serikali,” chanzo kimeeleza.
Njia ya pili ya kuhujumu mapato bandarini hapo, imetajwa kuwa ni ya kushirikiana na maafisa wa benki. Hii ina uhusiano mkubwa na njia ya kwanza inayohusisha matumizi ya mfumo wa malipo wa zamani usiokuwa wa kielektroniki.
Mfanyabiashara anaweza kuandikiwa kodi sahihi anayotakiwa kulipa, lakini anashirikiana na wafanyakazi wa benki anayokwenda kuweka fedha kwa kuhakikisha kuwa baada ya kufanikiwa kuondoa kontena bandarini, maafisa wa benki husika husitisha malipo hayo kwa kuondoa fedha husika kwa madai kuwa fedha ziliingizwa kwenye akaunti husika kimakosa.
“Huwa kuna ushirikiano wa karibu kati ya maafisa wa benki na mfanyabiashara husika. Baada ya kontena kutolewa bandarini, hamisho la fedha (transaction) huondolewa katika mfumo kwa maelezo kuwa halikuwa sahihi,” chanzo kimedai, huku kikisisitiza kuwa ushirikiano huo huhusisha pia watu wa Bandari na TRA ambao mwishowe hugawana malipo kadri wanavyokubaliana.
Tatu, ni mwanya wa uvushaji wa makontena yenyewe yasiyolipiwa ushuru kupitia mageti maalum yanayofahamika kwa kazi hiyo, hasa geti Namba 3 ambalo chanzo kimedai ndilo linaongoza kupitisha mizigo ya ‘dili’.
“Kwa ujumla yapo mageti matano ya kupitisha bidhaa mbalimbali, baadhi yakiwa ni ya kupitihia mafuta, nafaka na magari.
"Hili Namba 3 ndiyo hutumika kupitisha makontena ya bidhaa zenye thamani kubwa na wengi wasiolipa kodi hulitumia hili,” chanzo kilieleza kabla ya kufafanua kuwa awali, hilo geti Namba 3 halikuwa na mfumo wowote wa kuangalia kama kontena husika limelipiwa au la na ndiyo maana lilikuwa likitumika zaidi kupitisha makontena yasiyolipiwa kodi.
Njia ya nne ya kuhujumu kodi ya mapato ni ya kuwatumia watu wanaoendesha bandari kavu (ICD’s). Inaelezwa kuwa hivi sasa kuna bandari kavu 12, ambazo kila meli inapoingia hujulikana kila mzigo husika unapelekwa kwenye bandari ipi kati ya hizo.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kinachofanyika ni kwa baadhi ya makontena yanayotolewa bandarini ili yapelekwe bandari kavu kabla ya kukombolewa na wahusika huishia kupelekwa kwa wafanyabiashara wenye makontena na hivyo kuikosesha mapato serikali.
“Awali kwenye ICD’s kulikuwa na askari wa mmiliki wa ICD’s na siyo wa TPA… huyu alikuwa akiangalia malipo ya bosi wake tu ambayo ni gharama za kuhifadhi mzigo na hivyo TPA na TRA huambulia patupu,” chanzi kimeeleza, kikiongeza kuwa hivi sasa walau kuna nafuu kwani kwenye ICD’s kuna walinzi wa TPA lakini hilo limefanyika baada ya watu kuwa tayari wameshaiba sana.
Njia ya tano inayotumiwa kukwepa kodi ni ya kubadili taarifa, hasa kupitia watu wenye wajibu wa kufanya tathmini. Kwamba, badala ya mzigo kukadirwaa kodi kwa kiwango sahihi, wahusika ambao zaidi huwa ni watu wa TRA hukadiria fedha kidogo baada ya kujihakikishia kuwa nao wanapewa mgawo na wafanyabiashara.
“Hapo utakuta kontena la kodi ya milioni 80, mteja anaambiwa alipe milioni 40 tu … na wakati mwingine kiasi hicho pia hakiandikwi balki huandikwa cha chini zaidi kama milioni 5 tu…hii ni njia nyingine inayoligharimu taifa mabilioni ya fedha,” chanzo kimeeleza.
Njia ya sita inayofanikisha ukwepaji kodi ni mtandao mpana wa baadhi ya vigogo wa maeneo mbalimbali Bandarini na TRA, ambao hawa huhakikisha kuwa wanakuwa na timu ya vijana wao wa kazi karibu katika kila eneo ili kufanikisha mipango yao.
“Hii ndiyo njia kubwa ya hujuma. Kama utakumbuka aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisambaratisha baadhi ya mitandao kwa kuwagusa vigogo 27… ile ilikuwa kuvunja mtandao uliokuwapo. Hilo lilisaidia kiasi, lakini sasa ipo pia mitandao mingine ambayo uchunguzi ukifanyika utabaini kuwa mambo yameanza kurudi kama zamani,” imeelezwa.
Njia ya saba ya ukwepaji kodi ni kwa baadhi ya vigogo wa Bandari na TRA kuanzisha kampuni zao za uondoaji mizigo bandarini. Inaelezwa kuwa hizi hutumiwa sana kufanikisha ‘dili’ za ukwepaji kodi na ndiyo maana haishangazi kusikia kuwa kuna makontena zaidi ya 300 hayaonekani kwenye kumbukumbu za TRA.
Njia ya nane ya ukwepaji kodi ni kuonyesha kuwa kontena linapelekwa nje ya nchi, kwa mfano Malawi, wakati ukweli ni kwamba huishia hapahapa nchini.
“Utakuta kontena linadaiwa kupelekwa Malawi, lakini linachukuliwa na gari kukuu linaloonekana wazi kuwa haliwezi kufika hata Kibaha… njia hii pia hutumiwa sana kuikosesha serikali mapato,” chanzo kingine kilisema
Njia ya tisa ya ukwepaji kodi ni ucheleweshaji wa makusudi wa utoaji makontena. Kwamba, mteja anapotaka kutoa mzigo wake kwa kufuata njia halali zilizopo, huishia kuzungushwa kila uchao ili akubali kutoa rushwa na mwishowe kulipishwa kiwango pungufu cha kodi au kulipa fedha zisizoingia kabisa kwenye mikono ya TRA.
Njia ya kumi ni ubabaishaji unaofanyika katika kuorodhesha idadi ya makontena inayotolewa bandarini kwenda kwenye bandari kavu. Hapa, kama makontena yanayotolewa ni 12, basi huandikwa kuwa ni 10 na mengine mawili huishia kuondolewa bila ya kuwa na kumbukumbu zake kwa ajili ya kulipiwa kodi.
Pamoja na kuwapo kwa njia zote hizo, chanzo kimedai kuwa sababu kubwa ya kufanikiwa kwa ukwepaji kodi ni mtandao mpana unaoundwa na vigogo mbalimbali na ndiyo maana taarifa mbalimbali za wakaguzi wa ndani na wa nje katika Bandari ya Dar es Salaam huishia kubaki kwenye makabrasha bila ya kuwapo kwa utekelezaji wowote wa vitendo juu ya yale yanayopendekezwa na wataalamu.
Chanzo: Nipashe
0 comments: