SIRI
nje! Sakata la mmiliki wa Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan iliyopo
Ilala Bungoni, Dar, Dk. Juma Mwaka ‘JJ Mwaka’ kufanyiwa ziara ya
kushtukiza na baadaye kudaiwa kumkimbia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla limechukua sura
mpya huku mambo mengi yaliyomponza yakifichuka, Risasi
Jumamosi limechimba.
Dk. Kigwangalla akiingia kwenye Kliniki ya Tiba Asilia ya Fore Plan.
SOO LILIVYOKUWA
Siku
chache baada ya kuteuliwa kuwa naibu waziri, Dk. Kigwangalla alifanya
ziara ya kushtukiza katika kituo hicho kinachosifika kwa kutoa tiba ya
asili badala ya hospitali (tiba mbadala), hasa kwa wanawake
wanaosumbuliwa na matatizo ya uzazi.
Katika hali ya
kushangaza, matatibu na manesi waliokuwa kazini walitokomea
kusikojulikana na kuwatelekeza wagonjwa, wakikwepa kuonana na waziri
huyo ambaye akiwa na msafara wake, walifanya ukaguzi wa kina kwenye
kituo hicho.
Kufuatia kitendo cha Dk. Mwaka na
wenzake kuingia mitini, Waziri Kigwangalla alitoa amri ya kufungwa kwa
muda kwa kituo hicho mpaka uchunguzi wa kina utakapokamilika ili kuona
kama huduma zinazotolewa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.
Nyumba ya Dokta Mwaka JJ
MITANDAO YAMCHOMA
Simulizi
ya jinsi tabibu huyo alivyosimamishwa kutoa huduma ili kupisha
uchunguzi na ukaguzi wa kina, inaanzia mbali ambapo kwa mujibu wa vyanzo
vyetu vya kuaminika, chokochoko kuhusu huduma zake zilianzia kwenye
mitandao ya kijamii.
“Kwa kipindi kirefu kulikuwa
na makundi mawili yanayoshindana kwenye mitandao ya kijamii. Kundi la
kwanza ni wale waliowahi kutibiwa katika kliniki hiyo na kufanikiwa
kupona matatizo yao.
“Hawa walikuwa wakimtetea
kwamba anatoa huduma sahihi lakini kundi jingine ni wale waliotibiwa na
kupoteza fedha nyingi bila kupona matatizo yaliyokuwa yakiwasumbua.
“Hawa
ndiyo waliochangia kwa kiasi kikubwa kuifumbua macho Serikali ya Rais
John Pombe Magufuli kwani walitaka dawa na huduma za Dk. Mwaka
zichunguzwe kwa vile walishapoteza imani naye,” kilisema chanzo chetu
makini kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Gari lake, ania ya Range Rover-Sport SE
KUANIKA MAISHA YAKE MTANDAONI
Kwa
mujibu wa chanzo kingine, tabia ya Dk. Mwaka kupenda kuanika maisha
yake kwenye mitandao ya kijamii ni suala jingine lililomponza na kufanya
watu waanze kutilia shaka utajiri wake.
“Unajua
Dk. Mwaka na mkewe wamekuwa wakiposti kwenye mitandao ya kijamii, hasa
Instagram picha za magari yao ya kifahari anayomiliki likiwemo Range
Rover-Sport SE na hekalu (jumba kubwa la ghorofa) analoishi, lipo Mbezi
(Dar).
“Pia walikuwa na kawaida ya kujisifia
wanaposafiri kwenda nje ya nchi kufanya shopping, hasa Dubai. Hicho pia
kimemponza sana maana watu walianza kufuatilia utajiri wao na pengine
ndiyo waliomchongea serikalini,” kilisema chanzo hicho kilicho karibu na
familia hiyo.
VIPINDI RUNINGANI
Sababu
nyingine inayotajwa na vyanzo vyetu kwamba imemponza tabibu huyo, ni
ile kawaida yake ya kuendesha vipindi kwenye runinga, akieleza huduma
anazozitoa kwa lengo la kupata wateja wengi.
“Unajua
Dokta Mwaka ndiye anayeongoza kwa kuwa na vipindi vingi vya runinga
kwenye televisheni mbalimbali nchini. Kama unavyojua kipindi kimoja cha
runinga kulipia kinagharimu fedha nyingi sana. Sasa watu wakawa
wanajiuliza anapata wapi fedha za kulipia gharama hizo? Ni kutoka kwa
wateja wake kweli?” kilisema chanzo chetu.
KUPUUZA AGIZO LA WIZARA
Pia, habari za ndani zinadai kuwa, mwaka jana wizara husika iliwaita wataalam wote wanaotoa tiba mbadala na kuwapa masharti.
Masharti
hayo ni kutovaa koti jeupe, kutoning’iniza shingoni chombo cha
kusikilizia mapafu/mapigo ya moyo (stethoscope) na kutojiita madaktari
wakitakiwa kutumia utambulisho wa tabibu masharti ambayo karibu wote
wameyapuuza.
KUNA KOSA KUJITANGAZA?
Katika
utafiti uliofanywa na gazeti hili na kutiliwa nguvu na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu imebainika
kwamba, kwa mujibu wa viapo wanavyokula madaktari na matabibu ni makosa
kujitangaza kwenye redio, runinga au mitandao kwa lengo la kuwavuta
wagonjwa.
“Changamoto iliyopo kwetu ni kwamba
matangazo wanayoyatoa ni kinyume na kanuni lakini tumebaini kwamba
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo inasimamia sekta ya
mawasiliano na utangazaji nchini ndiyo inayoruhusu. Tumejipanga kukutana
nao ili kujadili jambo hili,” alisema Mwalimu.
SIYO MARA YA KWANZA KUFUNGIWA
Tukio
hili la kusimamishwa kutoa huduma, si la kwanza kumtokea Dk. Mwaka
ambapo mwaka jana, maafisa kutoka wizara ya afya walifika kwenye kliniki
hiyo kwa kushtukiza, wakiwa wameongozana na waandishi wa habari na
kufanya ukaguzi ambapo kutokana na kutoridhishwa na mazingira
waliyoyakuta, walilazimika kuifunga kliniki hiyo kwa muda usiojulikana.
Hata hivyo, wiki kadhaa baadaye, Dk. Mwaka alifungua kesi mahakamani kupinga kufungiwa huko na kushinda kesi.
0 comments: