Friday, November 20, 2015

LIPUMBA: MAGUFULI ANAKABILIWA NA HALI NGUMU YA BAJETI

prof+Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba.
HATIMAYE aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF aliyejiuzulu uenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba ameibuka na kusema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli anakabiliwa na hali ngumu ya bajeti kwa kipindi kijacho cha miaka mitano.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar leo, Lipumba amesema Rais Magufuli anakabiliwa na mambo kadhaa yakiwemo ya hali ngumu ya bajeti ya serikali kufuatia taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwezi Oktoba 2015 kuonesha kuwa, mwaka wa fedha 2014/2015 serikali ilipanga kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 12,178 ikiwa sehemu kubwa ni makusanyo ya mapato ya Tanzania Revenue Authority (TRA).
Aidha aliendelea kufafanua kuwa, serikali ilikusanya shilingi bilioni 10,507 mapato halisi ukilinganisha na bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 1,671 sawa na 14% ya malengo ya bajeti.
Akaongeza kuwa, halmashauri za wilaya, miji na majiji zilitarajiwa kukusanya shilingi bilioni 458.5 lakini zilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 360.1 sawa na 78.5% ya malengo ya bajeti.
Alisema kwa upande wa misaada, bajeti ya shilingi bilioni 1,481 ilitolewa na upungufu ukiwa ni bilioni 457 sawa na asilimia 31 ya bajeti huku mikopo yenye masharti nafuu ya shilingi bilioni 1,000 ikifanikiwa kwa bilioni 859.
Kwa upande wa wanahabari waliomuuliza maswali kuhusu kurudia uchaguzi wa urais katika serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Lipumba alisema, Rais Magufuli anao uwezo wa kuishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutoa uamuzi wa kumtangaza mshindi wa urais na sio kurudia uchaguzi kama ilivyoamuliwa na mwenyekiti wa Tume.
“Kila kitu kiko wazi, mawakala walipata nakala za kila jimbo kwa majimbo yote 54, binafsi namuomba aishauri Zec itangaze matokeo halisi tofauti na kurudia uchaguzi,” alisema Lipumba.
Akizungumzia kasi ya Rais Magufuli, Pro.Lipumba alisema anaiunga mkono hasa kupitia kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ huku akisisitiza kauli hiyo kuendelea kuzaa matunda.
Akampongeza kwa ziara zake za kushitukiza akieleza kuwa zinazaa matunda huku akionesha mfano mzuri pale alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kujionea hali halisi ya mashine za CT Scan na MRI zikiwa mbovu na baada ya siku chache kuwa zimetengenezwa.
Hata hivyo alisisitiza kuwa ziara hizo hazitakuwa na tija kama bajeti ya maendeleo haitakidhi matatizo ya Watanzania kama vile afya bora, elimu, ajira, kupambana na rushwa, miundo mbinu na kilimo bora

Author:

0 comments: